Je ni kwanini utumie viungo kama iliki, mdalasini na kitunguu saumu?

  • Kulinda mwili na magonjwa ya uzee na kansa
  • Utajiri wa virutubisho
  • Uwezo wa kuua bakteria na kuzuia fangasi

‘Let food be thy medicine, and medicine be thy food

Kwa tafsiri ya kiswahili isiyo rasmi ‘Acha chakula kiwe dawa na dawa iwe ni chakula’.

Haya sio maneno yangu bali ni maneno maarufu ya mwanafizikia wa zamani wa Kigiriki Hippocrates, ambae pia amekua akijulikana kama baba wa dawa za kimagharibi. Kubwa zaidi alikua akihimiza watu kutumia vyakula tulivyo navyo kama dawa ya kujikinga na magonjwa mbalimbali. Duniani kote kuna aina nyingi sana ya vyakula na viungo mathalani hapa kwetu Tanzania tuna utajiri mkubwa wa mimea mbalimbali pamoja na ardhi kubwa na yenye rutuba hivyo tukizingatia na kuvijua vyakula vyenye afya na kuvitumia ipasavyo tutakua hatua moja mbele kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Fahamu aina ya viungo na mimea mbalimbali na faida zake. Viungo vyote utakavyoviona katika andiko hili jua vinapatikana hapa nyumbani katika masoko mbalimbali.

Kitunguu saumu (Garlic)Kwa uchunguzi wa hivi karibuni imefahamika kwamba kiungo hichi kina uwezo mkubwa wa kinga dhidi ya baridi (magonjwa ya kifua), kushusha shinikizo la damu, na kuweka sawa wingi wa lijamu (cholesterol) katika mwili (mafuta yanayopatikana katika seli mwili) ambayo hayatakiwi kuzidi sababu yanaweza kusababisha magonjwa ya moyo hivyo kitunguu saumu kina kazi ya kuweka sawa. Pia kiungo hiki kinatibu maambukizi ya bakteria na fangasi, pia kinazuia ongezeko la chembe sahani ambazo zinasababisha damu kuganda katika mishipa unashauriwa angalau ule kitunguu saumu punje moja kwa siku.

Karafuu (Clove) Ukiachana na sifa yake kuu ya kuongeza harufu nzuri katika chakula lakini kiungo hiki kina faida nyingi sana nitakuja kuongelea zaidi katika makala yake peke yake. Karafuu ina wingi wa viuasumu mwilini (antioxidants) ambayo inasaidia kutokua na muendelezo wa magonjwa ya muda mrefu, inaweza kusaidia kujikinga na kansa mfano ina uwezo mkubwa wa kusaidia kusimamisha ukuaji wa uvimbe (tumor) kwa kuua seli za kansa. Pia karafuu inasaidia kuu bakteria mfano bakteria aina ya E.coli ambaye anasababisha sumu katika chakula (food poison). Zaidi pia inaimarisha afya ya ini, afya ya kinywa, inaweka sawa sukari katika damu, afya ya mifupa na kusaidia kupunguza wingi wa vidonda vya tumbo.

Iliki (Cardamom) Ushawahi kula wali wenye iliki? kama bado basi nakushauri siku moja ujaribu. Pamoja na kua kiungo muhimu katika vyakula iliki pia inasaidia sana kurahisisha mmengényo wa chakula na kuzuia matatizo ya gesi, inaondoa kiungulia, inasaidia kuondoa pumu hatua za awali. Pia Iliki ikichanganywa na mdalasini inasaidia kuondoa maumivu ya koo. Kiungo hiki kimekua kikitumika kama dawa kwa muda mrefu sana iliki pia kuongeza wingi wa oksigeni na kupumua vizuri. Zaidi pia kinaweza kusaidia katika safari ya kupunguza mwili. Kitu kingine muhimu inasemekana kwamba iliki ina uwezo mkubwa wa kuweka sawa hisia zetu ndio maana ‘wanaume wengi wa Pwani hawana hasira’ (hakuna uthibitisho wa kisayansi) ila tupe maoni yako.

Manjano (Turmeric) Kiungo hichi muhimu kina faida kubwa katika mwili na ubongo. Manjano inakemikali muhimu iitwayo curcumin ambayo inasaidia kupunguza aina mbalimbali za uvimbe, inapunguza maumivu katika mwili na miwasho. Manjano pia inawezo mkubwa wa kuchelewesha magonjwa ya uzee na ubongo kama Alzheimer’s. Inaongeza kumbukumbu – japo bado chunguzi mbalimbali zinaendelea. Inaondoa hatari ya magonjwa ya moyo inasaidia kujikinga na kansa.

Mdalasini (Cinnamon) Kiungo hiki sio kwamba tu kinaleta harufu na ladha nzuri katika chakula lakini pia kina faida nyingi katika afya ya mwanadamu. Inasaidia afya ya ngozi, afya ya kinywa, inapunguza dalili za mzio (allergy), inasaidia kupunguza matumizi ya sukari mathalani katika chai sababu ya ladha yake. Pia ina wingi wa viuasumu mwilini ambavyo vinasaidia kuzuia magonjwa mbalimbali. Lakini pia inauwezo mkubwa wa kuua bakteria na fangasi kama (candida). Lakini pia inauwezo wa kusaidia kuzuia virusi vya magonjwa kama homa ya dengu, mafua na hata VVU (japo jambo hili bado linafanyiwa utafiti na linahitaji matumizi zaidi ya kiungo hiki kupata uhakika.

Giligilani (Coriander) Wengi wanaijua giligilani kwa harufu nzuri katika chakula ila ina faida nyingine kama kuleta au kuongeza hamu ya chakula, inaondoa maumivu ya tumbo na kuvimbiwa. Pia inasaida kuweka sawa sukari katika damu, afya ya ngozi. Pia inasaidia kutoa uchafu katika mwili, inazuia magonjwa ya macho na kutibu chunusi.

Pilipili Manga (Black Pepper) Kiungo hiki ni maarufu sana duniani kote na zaidi hutumika katika vyakula vingi hivyo sio kiungo chakukosa jikoni kwako. Pilipili manga ina uwezo mkubwa wa kupunguza hamu ya kula na hivyo kuweza kudhibiti uzito mkubwa. Inasaidia katika mmengényo wa chakula na afya utumbo, inasaidia kuongeza kinga mwili. Pia ina vitutubisho vingi ina vitamin K, E,A ina madini ya kutosha kama zinc, calcium, potassium,iron,copper lakini zaidi ina manganese ambayo inasaidia afya ya mifupa.

Je kiungo kipi kati ya hivyo faida zake zimekuvutia tuandikie kwenye comment na endelea kua nasi pamoja katika blog yako pendwa ya Upawa kwa habari za afya na vyakula mbalimbali. Hivi ni baadhi tu ya viungo katika vingi vilivyopo tutaendelea kujifunza zaidi na zaidi.

Leave a comment